Kiini cha Mwili Ulio na Mungu
Mwenyezi Mungu alisema, Mungu mwenye mwili wa kwanza Aliishi duniani kwa miaka thelathini na tatu na nusu, lakini Alitekeleza huduma Yake kwa miaka mitatu na nusu pekee ya hiyo miaka yote. Kipindi Alichofanya kazi na kabla Aanze kazi Yake, Alikuwa na ubinadamu wa kawaida. Aliishi na ubinadamu Wake wa kawaida kwa miaka thelathini na tatu na nusu. Katika miaka yote mitatu na nusu ya mwisho Alijifichua kuwa Mungu mwenye mwili.
Kabla Aanze kutekeleza kazi ya huduma Yake, Alikuwa na ubinadamu wa kawaida, bila kuonyesha ishara ya uungu Wake, na ni baada tu ya kuanza rasmi kutekeleza huduma Yake ndipo uungu Wake uliwekwa wazi. Maisha na kazi Zake katika ile miaka ishirini na tisa yote ilidhihirisha kuwa Alikuwa mwanadamu halisi, mwana wa Adamu, mwili; kwani huduma Yake ilianza tu kwa dhati baada ya umri wa miaka ishirini na tisa. Maana ya kupata mwili ni kwamba Mungu Anajionyesha katika mwili, na Anakuja kufanya kazi miongoni mwa wanadamu wa uumbaji Wake katika umbo la mwili. Hivyo, ili Mungu kuwa mwili, ni lazima kwanza Apate umbo la mwili, mwili wenye ubinadamu wa kawaida; hili, angalau, ni lazima liwe ukweli. Kwa kweli, maana ya kupata mwili kwa Mungu ni kwamba Mungu Anaishi na kufanya kazi katika mwili, Mungu katika kiini Chake Anakuwa mwili, Anakuwa mwanadamu. Maisha Yake ya kimwili na kazi vinaweza kugawanywa katika hatua mbili. Kwanza ni maisha Anayoishi kabla ya kuanza kutekeleza huduma Yake. Anaishi katika familia ya kawaida ya binadamu, katika ubinadamu wa kawaida kabisa, Akifuata maadili na sheria za maisha ya wanadamu, Akiwa na mahitaji ya kawaida ya binadamu (chakula, nguo, makazi, na usingizi), na udhaifu wa kawaida wa binadamu na hisia za kawaida za binadamu. Kwa maneno mengine, katika hatua hii ya kwanza Anaishi maisha yasiyo na uungu, ubinadamu wa kawaida kabisa, Akijishughulisha na shughuli zote za wanadamu. Hatua ya pili ni ya maisha Anayoishi baada ya kuanza kutekeleza huduma Yake. Bado Yumo katika ubinadamu wa kawaida Akiwa na umbo la nje la binadamu bila kuonyesha ishara isiyo ya kawaida kwa nje. Lakini kimsingi Anaishi kwa ajili ya huduma Yake, na wakati huu ubinadamu Wake wa kawaida upo kikamilifu kuhudumia kazi ya kawaida ya uungu Wake; kwani wakati huo, ubinadamu Wake wa kawaida umekomaa kiasi cha kuweza kutekeleza huduma Yake. Kwa hivyo hatua ya pili ya maisha Yake ni ya kutekeleza huduma Yake katika ubinadamu Wake wa kawaida, ni maisha ya ubinadamu wa kawaida na uungu kamili. Sababu ya kuishi katika maisha ya kawaida kabisa ya ubinadamu katika hatua ya kwanza ya maisha Yake ni kwamba ubinadamu Wake bado ulikuwa haujalingana na ukamilifu wa kazi ya uungu, bado haujakomaa; ni baada tu ya kukomaa kwa ubinadamu Wake na kuwa na uwezo wa kustahimili huduma Yake, ndipo Anaweza kuanza kutekeleza huduma Yake. Kwa kuwa Yeye, kama mwili, Anahitaji kukua na kukomaa, hatua ya kwanza ya maisha Yake ni ile ya ubinadamu wa kawaida, ilhali katika hatua ya pili, kwa kuwa ubinadamu Wake una uwezo wa kuanza kazi Yake na kutekeleza huduma Yake, maisha ambayo Mungu mwenye mwili Anaishi katika kipindi cha huduma Yake ni ya ubinadamu na ya uungu kamili. Iwapo Mungu mwenye mwili Angeanza huduma Yake kwa dhati tangu kuzaliwa kwake, na kufanya ishara na maajabu ya mwujiza, basi Asingekuwa na kiini cha kimwili. Kwa hivyo, ubinadamu Wake upo kwa sababu ya kiini chake cha Kimwili; hakuwezi kuwepo na mwili bila ubinadamu, na mtu bila ubinadamu si mwanadamu. Kwa njia hii, ubinadamu wa mwili wa Mungu ni sifa ya ndani ya mwili wa Mungu. Kusema kwamba “Mungu Anapokuwa mwili Anakuwa na uungu kamili, kwa vyovyote vile si ubinadamu,” ni kufuru, kwa sababu huu ni msimamo usioweza kuchukuliwa, msimamo unaokinzana na kanuni ya Yesu kuupata mwili. Hata baada ya kuanza kutekeleza huduma Yake, uungu Wake bado unaishi ndani ya umbo la nje la binadamu Anapofanya kazi Yake; ni kwamba tu wakati huo, ubinadamu Wake una kusudi la pekee la kuuwezesha uungu Wake kutekeleza kazi katika mwili wa kawaida. Kwa hivyo wakala wa kazi ni uungu unaosetiriwa katika ubinadamu Wake. Ni uungu na wala si ubinadamu Wake unaofanya kazi, lakini ni uungu uliojificha katika ubinadamu Wake; kimsingi kazi Yake inafanywa na uungu Wake kikamilifu, haifanywi na ubinadamu Wake. Ila mtekelezaji wa kazi ni mwili Wake. Mtu anaweza kusema kuwa Yeye ni mwanadamu na vilevile Mungu, kwani Mungu Anakuwa Mungu Anayeishi katika mwili, mwenye umbo la mwanadamu na kiini cha binadamu lakini pia na kiini cha Mungu. Kwa sababu ni mwanadamu mwenye kiini cha Mungu, Yuko juu ya wanadamu wote walioumbwa, juu ya mwanadamu yeyote anayeweza kutekeleza kazi ya Mungu. Kwa hivyo, miongoni mwa wale wote walio na umbo la binadamu kama Lake, miongoni mwa wale wote walio na ubinadamu, Yeye pekee ndiye Mungu mwenye mwili Mwenyewe—wengine wote ni wanadamu walioumbwa. Japokuwa wote wana ubinadamu, wanadamu walioumbwa si chochote zaidi ya wanadamu, ilhali Mungu mwenye mwili ni tofauti: katika mwili Wake, si tu kwamba ana ubinadamu ila pia muhimu zaidi Ana uungu. Ubinadamu Wake waweza kuonekana katika mwonekano wa nje wa Mwili Wake na katika maisha Yake ya kila siku; ila uungu Wake ni vigumu kuonekana. Kwa kuwa uungu Wake huonyeshwa pale tu Anapokuwa na ubinadamu, na si wa kimuujiza kama watu wanavyoukisia kuwa, ni vigumu sana kwa watu kuuona. Hata leo hii ni vigumu sana kwa watu kuelewa kiini cha kweli cha Mungu mwenye mwili. Kwa kweli, hata baada ya Mimi kulizungumzia kwa mapana, Natarajia bado liwe fumbo kwa wengi wenu. Suala hili ni rahisi sana: kwa kuwa Mungu Anakuwa mwili, kiini Chake ni muungano wa ubinadamu na uungu. Muungano huu unaitwa Mungu Mwenyewe, Mungu Mwenyewe duniani.
Maisha Aliyoishi Yesu duniani yalikuwa maisha ya kimwili ya kawaida. Aliishi katika ubinadamu wa kawaida wa mwili Wake. Mamlaka Yake—kufanya kazi Yake na kuzungumza neno Lake, au kuwaponya wagonjwa au kufukuza mapepo, kufanya hiyo kazi isiyo ya kawaida—hayakujitokeza, kwa kiasi kikubwa, hadi Alipoanza huduma Yake. Maisha Yake kabla ya umri wa miaka ishirini na tisa, kabla ya Yeye kuanza kutekeleza huduma Yake, yalikuwa uthibitisho tosha kuwa Alikuwa mwili wa kawaida. Kwa sababu ya hili, na kwa kuwa Alikuwa bado Hajaanza kutekeleza huduma Yake, watu hawakuona chochote cha uungu ndani Yake, hawakuona chochote zaidi ya ubinadamu wa kawaida, mwanadamu wa kawaida—kama vile wakati ule baadhi ya watu walimwamini kuwa mwana wa Yosefu. Watu walidhani kuwa Alikuwa mwana wa mwanadamu wa kawaida, hawakuwa na njia ya kugundua kuwa Alikuwa mwili wa Mungu; hata wakati Alipotenda miujiza mingi katika harakati za kutekeleza huduma Yake, watu wengi bado walisema Alikuwa mwana wa Yosefu, kwani Alikuwa Kristo mwenye umbo la nje la ubinadamu wa kawaida. Ubinadamu Wake wa kawaida pamoja na kazi yake vyote vilikuwepo ili kutimiza umuhimu wa kupata mwili kwa mara ya kwanza, kuthibitisha kuwa Mungu Alikuwa Amekuja katika mwili kwa ukamilifu, kuwa mwanadamu wa kawaida kabisa. Kuwa na ubinadamu wa kawaida kabla ya kuanza kazi Yake ulikuwa uthibitisho kuwa Alikuwa mwili wa kawaida; na kwa kuwa Alifanya kazi baadaye lilithibitisha pia kuwa Alikuwa mwili wa kawaida, kwa kuwa Alifanya ishara na miujiza, kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo katika mwili na ubinadamu wa kawaida. Sababu za kufanya miujiza ilikuwa kwamba mwili Wake ulikuwa umebeba mamlaka ya Mungu, ulikuwa mwili ambamo Roho wa Mungu Alikuwa Amesetiriwa. Alikuwa na mamlaka haya kwa sababu ya Roho wa Mungu, na haikumaanishi kuwa Hakuwa Mwili. Kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo ilikuwa kazi Aliyopaswa kutekeleza katika huduma Yake, onyesho la uungu Wake uliojificha ndani ya ubinadamu Wake, na haijalishi ni ishara za aina gani Alionyesha au Alidhihirisha vipi mamlaka Yake, bado Aliishi katika ubinadamu wa kawaida na bado Alikuwa mwili wa kawaida. Aliishi katika mwili wa kawaida mpaka wakati Alipofufuliwa baada ya kufa msalabani. Aliishi katika mwili wa kawaida. Akitoa neema, Akiwaponya wagonjwa, na kufukuza mapepo hayo yote yalikuwa sehemu ya huduma Yake, hiyo yote ilikuwa kazi Aliyotekeleza katika mwili Wake wa kawaida. Kabla ya kwenda msalabani, Hakuuacha mwili Wake wa kawaida, haijalishi Alikuwa Anafanya nini. Alikuwa Mungu Mwenyewe, Akifanya kazi ya Mungu, lakini kwa sababu Alikuwa Mwili wa Mungu, Alikula chakula na kuvaa nguo, Alikuwa na mahitaji ya kawaida ya binadamu, Alikuwa na fikira za kawaida za binadamu na akili za kawaida. Haya yote yalikuwa uthibitisho kwamba Alikuwa mwanadamu wa kawaida, ambayo yalithibitisha kuwa mwili wa Mungu ulikuwa mwili wenye ubinadamu wa kawaida, haukuwa wa rohoni. Kazi Yake ilikuwa kukamilisha kazi ya Mungu kupata mwili mara ya kwanza, kutimiza huduma ya kupata mwili mara ya kwanza. Umuhimu wa kupata mwili ni kwamba mtu wa kawaida Anatekeleza kazi ya Mungu Mwenyewe; yaani, kwamba Mungu Anatekeleza kazi Yake ya uungu katika ubinadamu na hivyo kumshinda Shetani. Kupata mwili kunamaanisha kwamba Roho wa Mungu Anakuwa Mwili, yaani, Mungu Anakuwa mwili; kazi Anayoifanya katika mwili ni kazi ya Roho, inayothibitika katika mwili, na kuonyeshwa kwa mwili. Hakuna mwingine ila tu mwili wa Mungu Anayeweza kutimiza huduma ya Mungu mwenye mwili; yaani, mwili wa Mungu kuwa mwili pekee, ubinadamu huu wa kawaida—na hakuna mwingine yeyote—anayeweza kuonyesha kazi ya uungu. Ikiwa, wakati wa kuja Kwake wa kwanza, Mungu Asingekuwa Amekuwa na ubinadamu wa kawaida kabla ya umri wa miaka ishirini na tisa—ikiwa mara tu Alipozaliwa Angeweza kufanya miujiza, ikiwa mara tu Alipojifunza kuongea Angeweza kuongea lugha ya mbinguni, ikiwa mara tu Alipokanyaga duniani Angeweza kuyaelewa mambo yote ya kidunia, kung’amua fikira za kila mtu na nia zao—mtu kama huyu asingeitwa mwanadamu wa kawaida, na mwili Wake usingeitwa mwili wa mwanadamu. Iwapo mambo yangekuwa hivi kwa Kristo, basi maana na kiini cha kuwa mwili kwa Mungu ingepotea. Kuwa Kwake na ubinadamu wa kawaida kunathibitisha kuwa Alikuwa Mungu Aliyejidhihirisha katika mwili; ukweli kwamba Alipitia ukuaji wa kawaida wa binadamu unaonyesha zaidi kuwa Alikuwa mwili wa kawaida; na zaidi, kazi Yake ni uthibitisho tosha kuwa Alikuwa Neno la Mungu, Roho wa Mungu, kuwa mwili. Mungu Anakuwa mwili kwa sababu ya mahitaji ya kazi; kwa maneno mengine, hii hatua ya kazi inapaswa kufanywa kwa mwili, kufanywa katika ubinadamu wa kawaida. Hili ndilo sharti la “Neno kuwa mwili,” la “Neno kuonekana katika mwili,” na ndio ukweli wa Mungu kupata mwili mara Mbili. Watu huenda wakaamini kuwa maisha yote ya Yesu yaliambatana na miujiza, kwamba hadi mwisho wa kazi Yake duniani Hakudhihirisha ubinadamu wa kawaida, kwamba Hakuwa na mahitaji ya kawaida ya mwanadamu au udhaifu au hisia za binadamu, kwamba Hakuhitaji vitu vya kimsingi vya maisha au kuwa na fikira za kawaida za binadamu. Wanadhani tu kuwa Alikuwa mwanadamu asiyekuwa na akili ya kawaida, aliyevuka mipaka ya ubinadamu. Wanaamini kuwa kwa sababu Yeye ni Mungu, Hapaswi kufikiri na kuishi jinsi wanadamu wa kawaida hufanya, kwamba ni mtu wa kawaida tu, mwanadamu halisi, anayeweza kufikiri fikira za mwanadamu wa kawaida na kuishi maisha ya mwanadamu wa kawaida. Haya yote ni mawazo ya wanadamu na maoni ya wanadamu, ambayo yanakinzana na madhumuni asilia ya kazi ya Mungu. Kufikiri kwa mwanadamu wa kawaida kunadumisha mawazo ya kawaida ya mwanadamu na ubinadamu wa kawaida; ubinadamu wa kawaida unadumisha kazi za kawaida za mwili; na kazi za kawaida za mwili zinawezesha maisha ya kawaida ya mwili katika ukamilifu wake. Ni kwa kufanya kazi tu katika mwili kama huo ndipo Mungu Anaweza kutimiza kusudi la kupata mwili Kwake. Kama Mungu mwenye mwili angekuwa na umbo la nje tu la mwili, bila kufikiri fikira za kawaida za binadamu, basi mwili huu usingekuwa na mawazo ya binadamu, sembuse ubinadamu halisi. Ni vipi ambavyo mwili kama huu, usio na ubinadamu, ungeweza kutimiza huduma ambayo Mungu mwenye mwili Anapaswa kutekeleza? Akili za kawaida huwezesha vipengele vyote vya maisha ya binadamu; bila akili ya kawaida, mtu hawezi kuwa mwanadamu. Kwa maneno mengine, mtu asiyefikiria fikra za kawaida ni mgonjwa wa akili. Na Kristo ambaye Hana ubinadamu ila uungu pekee Hawezi kuitwa mwili wa Mungu. Basi, mwili wa Mungu unawezaje kukosa ubinadamu wa kawaida? Je, si kufuru kusema kwamba Kristo hana ubinadamu? Kila shughuli ambazo wanadamu wa kawaida hufanya hutegemea utendaji kazi wa akili ya kawaida ya mwanadamu. Bila hiyo, wanadamu wangekuwa na mienendo iliyopotoka; wangeshindwa hata kutofautisha kati ya nyeupe na nyeusi, wema na uovu; na hawangekuwa na maadili ya binadamu na kanuni za uadilifu. Vivyo hivyo, iwapo Mungu mwenye mwili Asingefikiri kama mwanadamu wa kawaida, basi Asingekuwa mwili halisi, mwili wa kawaida. Mwili usiofikiri kama huo haungeweza kuikabili kazi ya uungu. Haungeweza kushiriki katika shughuli za kawaida za kimwili, wala hata kuishi na wanadamu duniani. Hivyo basi, umuhimu wa Mungu kupata mwili, kiini kabisa cha Mungu kuja duniani, kingepotea. Ubinadamu wa Mungu kuwa mwili huwepo kudumisha kazi ya kawaida ya uungu katika mwili; fikira Zake za kawaida za binadamu zinadumisha ubinadamu Wake wa kawaida na shughuli Zake zote za kimwili. Mtu anaweza kusema kuwa fikira zake za kawaida za binadamu zipo ili kudumisha kazi yote ya Mungu katika mwili. Kama mwili huu usingekuwa na akili ya mwanadamu wa kawaida, basi Mungu Asingefanya kazi katika mwili, na Anachopaswa kufanya kimwili kisingetimilika. Japo Mungu mwenye mwili Ana akili ya mwanadamu wa kawaida, kazi Yake haijatiwa doa na mawazo ya binadamu; Anafanya kazi katika ubinadamu na akili ya kawaida chini ya masharti ya awali kuwa atakuwa na ubinadamu na akili ya kawaida, na si na mawazo ya kawaida ya binadamu. Haijalishi mawazo ya mwili Wake ni bora kiasi gani, kazi Yake haionyeshi alama ya mantiki au kufikiria. Kwa maneno mengine, kazi Yake haiwazwi na akili ya mwili Wake, ila ni onyesho la moja kwa moja la kazi ya uungu katika ubinadamu Wake. Kazi Yake yote ni huduma Anayostahili kutimiza, na haiwazwi hata chembe kwa akili Zake. Kwa mfano, kuponya wagonjwa, kufukuza mapepo na kusulubishwa hayakuwa mazao ya akili Zake za binadamu, yasingeweza kutimizwa na mwanadamu yeyote mwenye akili za binadamu. Vivyo hivyo, kazi ya ushindi ya leo ni huduma ambayo ni sharti itekelezwe na Mungu mwenye mwili, lakini si kazi ya mapenzi ya mwanadamu, ni kazi ambayo uungu Wake unapaswa kufanya, kazi ambayo hakuna mwanadamu wa mwili anaiweza. Kwa hivyo, Mungu mwenye mwili ni lazima Awe na akili za binadamu, ni lazima Awe na ubinadamu wa kawaida, kwa sababu ni lazima Atekeleze kazi Yake katika ubinadamu akiwa na akili za kawaida. Hiki ndicho kiini cha kazi ya Mungu mwenye Mwili, kiini chenyewe cha Mungu mwenye mwili.
Kabla Yesu Hajatekeleza kazi yake, Aliishi tu katika ubinadamu Wake wa kawaida. Hakuna mtu ambaye angeweza kutambua kuwa Alikuwa Mungu, hakuna aliyegundua kuwa Alikuwa Mungu mwenye mwili; watu walimjua tu kama mwanadamu wa kawaida kabisa. Ubinadamu Wake wa kawaida ulikuwa uthibitisho kuwa Mungu Alipata mwili, na kwamba Enzi ya Neema ilikuwa enzi ya kazi ya Mungu mwenye mwili, si enzi ya kazi ya Roho. Ilikuwa uthibitisho kuwa Roho wa Mungu Alipatikana kikamilifu katika mwili, kwamba katika enzi ya kupata mwili kwa Mungu mwili Wake ungetekeleza kazi yote ya Roho. Kristo mwenye ubinadamu wa kawaida ni mwili ambao kwao Roho Hupatikana, Akiwa na ubinadamu wa kawaida, ufahamu wa kawaida, na fikira za wanadamu. “Kupatikana” kunamaanisha Mungu kuwa mwanadamu, Roho kuwa mwili; kuiweka wazi, ni wakati ambapo Mungu Mwenyewe Anaishi katika mwili wenye ubinadamu wa kawaida, na kupitia kwenye huo mwili, Anaonyesha kazi yake ya uungu—hii ndiyo maana ya kupatikana, au kupata mwili. Wakati wa kupata mwili Kwake mara ya kwanza, ilikuwa muhimu kwa Mungu kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo kwa sababu kazi Yake ilikuwa ni kukomboa. Ili kulikomboa kabila lote la mwanadamu, Alipaswa kuwa mwenye upendo na mwenye kusamehe. Kazi Aliyoifanya kabla ya kusulubiwa ilikuwa kuponya watu na kufukuza mapepo, ambayo iliashiria wokovu Wake wa mwanadamu kutoka katika dhambi na uchafu. Kwa sababu ilikuwa ni Enzi ya Neema, ilikuwa muhimu Kwake kuponya wagonjwa, na kwa njia hiyo Alionyesha ishara na miujiza, mambo ambayo yalikuwa kiwakilishi cha neema katika hiyo enzi; kwani Enzi ya Neema ilikitwa katika kutolewa kwa neema, ikiashiriwa na amani, furaha, na baraka ya vitu, vyote vikiwa zawadi za imani ya watu kwa Yesu. Hii ni kusema kuwa, kuponya wagonjwa, kufukuza mapepo na kutoa neema ulikuwa uwezo asilia wa mwili wa Yesu katika Enzi ya Neema, mambo haya yalikuwa ni kazi ya Roho iliyopatikana katika mwili. Lakini Alipokuwa Akitekeleza kazi kama hiyo, Alikuwa Akiishi katika mwili, Hakuenda nje ya mipaka ya mwili. Haijalishi ni matendo gani ya uponyaji Aliyotekeleza, bado Alikuwa na ubinadamu wa kawaida, bado Aliishi maisha ya kawaida ya binadamu. Sababu inayonifanya Niseme kuwa katika enzi ya kupata mwili kwa Mungu mwili ulitekeleza kazi yote ya Roho, ni kuwa haijalishi ni kazi gani Aliyoifanya, Aliifanya katika mwili. Lakini kwa sababu ya kazi Yake, watu hawakuchulia mwili Wake kuwa ulikuwa na kiini cha kimwili, kwani huu mwili ungefanya maajabu, na baadhi ya nyakati maalum ungefanya mambo ambayo yalivuka uwezo wa kimwili. Kwa hakika, haya matukio yote yalitokea Alipoanza huduma Yake, kama vile Yeye kujaribiwa kwa siku arobaini au kubadilishwa kule mlimani. Hivyo kwa Yesu, maana ya kupata mwili kwa Mungu haikukamilishwa, ila tu sehemu yake ilitimizwa. Maisha Aliyoishi katika mwili kabla ya kuanza kazi Yake yalikuwa ya kawaida tu katika hali zote. Alipoanza kazi Alidumisha umbo la nje la mwili Wake tu. Kwa sababu kazi Yake ilikuwa onyesho la uungu Wake, ilipita kazi ya kawaida ya mwili. Hata hivyo, Mwili wa Mungu ulikuwa tofauti na wanadamu wenye nyama na damu. Kwa hakika, katika maisha Yake ya kila siku, Alihitaji chakula, nguo, usingizi, na makao kama mtu yeyote yule, Alikuwa na mahitaji ya lazima ya kawaida, Alifikiri na kuwaza kama mwanadamu wa kawaida. Bado watu walimchukulia kuwa mwanadamu wa kawaida, isipokuwa tu kwamba kazi Aliyoifanya ilikuwa ya kupita akili. Kwa hakika, haijalishi Alifanya nini, Aliishi katika ubinadamu wa kawaida, na hata Alipotekeleza kazi, fikira zake zilikuwa za kawaida, mawazo yake yalikuwa ya wazi, hata zaidi ya wanadamu wa kawaida. Ilikuwa muhimu kwa Mungu mwenye mwili kufikiri kwa njia hii, kwani kazi ya uungu ilipaswa ionyeshwe na mwili ambao fikira zake zilikuwa za kawaida sana na mawazo yake wazi kabisa—ni kwa njia hii tu ndiyo mwili Wake ungeweza kuonyesha kazi ya uungu. Wakati wote wa miaka yote thelathini na tatu na nusu ambayo Yesu Aliishi duniani, Alidumisha ubinadamu Wake wa Kawaida, ila kwa sababu ya kazi Yake katika huduma Yake ya miaka mitatu na nusu, watu walidhani kuwa Alikuwa Amepita mipaka ya ubinadamu, kwamba Alikuwa wa rohoni zaidi kuliko hapo awali. Kwa kweli, ubinadamu wa kawaida wa Yesu haukubadilika kabla na baada ya Yeye kuanza huduma Yake; ubinadamu Wake ulikuwa sawa wakati wote, lakini kwa sababu ya tofauti kabla na baada ya Yeye kuanza huduma Yake, mitazamo miwili ilijitokeza kuhusiana na mwili Wake. Haijalishi watu walifikiria nini, Mungu mwenye mwili Alidumisha ubinadamu Wake asilia wa kawaida kipindi chote, kwani kwa sababu Mungu Alikuwa mwili, Aliishi katika mwili, mwili uliokuwa na ubinadamu wa kawaida. Hata ikiwa Alikuwa Anatekeleza huduma Yake au la, ubinadamu Wake wa kawaida usingeweza kufutika, kwani ubinadamu ndio kiini cha msingi cha mwili. Kabla Yesu hajaanza kutekeleza huduma Yake, mwili Wake ulibaki wa kawaida kabisa, ukishiriki katika shughuli zote za binadamu; Hakuonekana hata kidogo kuwa wa rohoni, Hakuonyesha ishara zozote za kimiujiza. Wakati ule Alikuwa tu mwanadamu wa kawaida sana Aliyemwabudu Mungu, japo dhamira Yake ilikuwa adilifu sana, ya kweli zaidi kuliko ya mtu yeyote. Hivi ndivyo ubinadamu Wake wa kawaida ulijionyesha wenyewe. Kwa kuwa Hakufanya kazi kabisa kabla ya kuianza huduma Yake, hakuna aliyemtambua, hakuna aliyegundua kuwa mwili Wake ulikuwa tofauti kabisa na miili ya watu wengine, kwa kuwa Hakutenda muujiza hata mmoja, Hakutenda hata chembe ya Kazi ya Mungu. Hata hivyo, baada ya kuanza kutekeleza kazi Yake, Alidumisha umbo la nje la ubinadamu wa kawaida na kuendelea kuishi katika mawazo ya kawaida ya binadamu, lakini kwa kuwa Alikuwa Ameanza kufanya kazi ya Mungu Mwenyewe, kuanzisha huduma ya Kristo na kufanya kazi ambayo wanadamu hai, wanadamu wenye nyama na damu, wasingeweza kufanya, basi watu walidhani kuwa Hakuwa na ubinadamu wa kawaida na Hakuwa mwili wa kawaida kikamilifu ila mwili usio kamili. Kwa sababu ya yale Aliyotekeleza, watu walisema kuwa Alikuwa Mungu katika mwili Ambaye Hakuwa na ubinadamu wa kawaida. Huu ulikuwa ufahamu wa kimakosa, kwani watu hawakuelewa maana ya Mungu kupata mwili. Huu ufahamu mbaya ulitokana na ukweli kuwa kazi iliyoonyeshwa na Mungu katika mwili ilikuwa kazi ya uungu, iliyoonyeshwa kupitia kwa mwili wenye ubinadamu wa kawaida. Mungu Alikuwa Amevishwa katika mwili, Alikaa ndani ya mwili, na kazi Yake katika ubinadamu Wake iliuziba ukawaida wa ubinadamu Wake. Kwa sababu hii, watu walidhani kuwa Mungu Hakuwa na ubinadamu.
Mungu mwenye mwili wa kwanza Hakukamilisha kazi ya kupata mwili; Alikamilisha tu hatua ya kwanza ya kazi iliyokuwa lazima kwa Mungu kuifanya katika mwili. Kwa hivyo, ili kuimaliza kazi ya kupata mwili, Mungu Amerudi katika mwili kwa mara nyingine tena, Akiishi kulingana na ukawaida na uhalisia wote wa mwili, yaani, kuifanya kazi ya Mungu ijitokeze katika mwili wa kawaida kabisa, na kwa njia hiyo Anahitimisha kazi Aliyoiacha bila kukamilisha katika mwili. Mwili wa pili uliopatikana kimsingi ni sawa na ule wa kwanza, lakini ni halisi zaidi, wa kawaida kabisa kuliko ule wa kwanza. Kwa sababu hiyo, mateso unayoyapitia mwili wa pili uliopatikana ni makubwa kuliko yale ya ule wa kwanza, ila mateso haya ni kwa sababu ya huduma Yake katika mwili, ambayo ni tofauti na mateso ya mwanadamu mwovu. Vilevile yanachipuka kutokana na ukawaida na uhalisi wa mwili Wake. Kwa kuwa Anatekeleza huduma Yake katika mwili wa kawaida na halisi kabisa, mwili ni sharti upitie mateso mazito. Kadiri mwili ulivyo wa kawaida na halisi, ndivyo unateseka zaidi katika utekelezaji wa huduma Yake. Kazi ya Mungu inaonyeshwa katika mwili wa kawaida sana, mwili ambao si wa rohoni kamwe. Kwa kuwa mwili Wake ni wa kawaida, na ni lazima ubebe kazi ya kumwokoa mwanadamu, Anateseka hata zaidi kuliko ambavyo mwili wa rohoni unaweza kuteseka—mateso haya yote yanatokana na uhalisi na ukawaida wa mwili Wake. Kutokana na mateso yaliyopitiwa na hii miili miwili iliyopatikana wakati wa kutekeleza huduma Zao, mtu anaweza kuona kiini cha mwili uliopatikana. Kadiri mwili ulivyo wa kawaida, ndivyo Anapata mateso mazito Afanyapo kazi, kadri mwili unaofanya kazi unavyokuwa wa kweli, ndivyo maoni ya watu yanaendelea kuwa makali, na hatari zinazomkabili zinaendelea kuongezeka. Lakini, kadiri mwili ulivyo halisi, kadiri mwili unavyokuwa na hali kamili ya binadamu wa kawaida, ndivyo Anaweza zaidi kuifanya kazi ya Mungu katika mwili. Ulikuwa mwili wa Yesu ulioangikwa msalabani, mwili Wake Alioutoa kama kafara kwa dhambi; ni kupitia kwa mwili wenye ubinadamu wa kawaida ndipo Aliweza kumshinda Shetani na kumkomboa kabisa mwanadamu kutoka msalabani. Ni kupitia mwili kamili ndipo Mungu katika mwili mara ya pili Anatekeleza kazi ya ushindi na kumshinda Shetani. Ni mwili tu wa kawaida na halisi kabisa unaoweza kutekeleza kazi ya ushindi kwa ukamilifu wake na kutoa ushuhuda wa nguvu. Hii ni sawa na kusema kwamba kazi ya[a] kumshinda mwanadamu inafanywa kuwa bora kupitia uhalisia na ukawaida wa mwili wa Mungu, si kupitia miujiza mikuu na ufunuo. Huduma ya huyu Mungu mwenye mwili ni ya kunena na kwa njia hiyo inamshinda mwanadamu na kumfanya mkamilifu; kwa maneno mengine, kazi ya Roho Aliyejitokeza katika mwili, wajibu wa mwili, ni kunena na kupitia kwa hili kumshinda, kumfichua, kumfanya kuwa kamilifu, na kumwondoa mwanadamu kabisa. Kwa hivyo, ni katika kazi ya kushinda ambapo kazi ya Mungu katika mwili itatimiziwa kwa ukamilifu. Kazi ya ukombozi ya kwanza ilikuwa mwanzo tu wa kazi ya kupata mwili kwa Yesu; mwili unaofanya kazi ya kushinda utaikamilisha kazi nzima ya kupata mwili kwa Yesu. Kijinsia, mmoja ni mwanamke na mwingine ni mwanamume; kwa hili, maana ya kupata mwili kwa Mungu imekamilishwa. Mawazo mabaya ya mwanadamu kumhusu Mungu yameondolewa: Mungu Anaweza kuwa mwanamke na mwanamume, na kimsingi Mungu mwenye mwili Hana jinsia. Alimuumba mwanamume na mwanamke, na Hatofautishi kati ya hizi jinsia. Katika hatua hii ya kazi, Mungu Hafanyi ishara na miujiza, ili kwamba kazi iweze kutimiza matokeo yake kupitia kwa maneno. Sababu ya jambo hili, aidha, ni kwa maana kazi ya Mungu mwenye mwili mara hii si kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo, ila kumshinda mwanadamu kupitia kunena, ikiwa na maana kwamba uwezo asili uliomo kwenye huu mwili uliopatikana wa Mungu ni kunena maneno na kumshinda mwanadamu, si kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo. Kazi Yake katika ubinadamu wa kawaida si kutenda miujiza, si kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo, ila ni kunena, na kwa hivyo Yesu kupata mwili kwa mara ya pili kunaonekana kwa watu kuwa kawaida zaidi ya mara ya kwanza. Watu wanaona kuwa Mungu kupata mwili si uongo; lakini huyu Mungu mwenye mwili ni tofauti na Yesu Aliyekuwa mwili, na japo wote ni Mungu wenye mwili, Hawako sawa kabisa. Yesu Alikuwa na ubinadamu wa desturi, ubinadamu wa kawaida, lakini Aliambatana na ishara nyingi na miujiza. Katika huyu Mungu mwenye mwili, macho ya mwanadamu hayataona ishara au miujiza, wala kuponya wagonjwa au kufukuza mapepo, wala kutembea juu ya bahari, wala kufunga kwa siku arobaini… Hafanyi kazi sawa na Aliyoifanya Yesu, si kwa kuwa mwili Wake kimsingi ni tofauti na ule wa Yesu, ila ni kwa sababu si huduma Yake kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo. Haharibu kazi Yake mwenyewe, Havurugi kazi Yake mwenyewe. Kwa kuwa anamshinda mwanadamu kwa maneno Yake halisi, haina haja ya kumhini kwa miujiza, na kwa hivyo hii hatua ni kukamilisha kazi ya kupata mwili. Mungu mwenye mwili umwonaye leo ni mwili kabisa, na hana hali ya rohoni ndani yake. Anakuwa mgonjwa sawa tu na watu wengine, Anahitaji chakula na nguo sawa tu na watu wengine, kwani ni mwili kabisa. Ikiwa wakati huu Mungu mwenye mwili Angetekeleza ishara na miujiza mikuu, ikiwa Angeponya wagonjwa, kufukuza mapepo, au Angeweza kuua kwa neno moja tu, kazi ya kushinda ingefanywaje? Kazi ingeenezwa vipi miongoni mwa watu wa Mataifa? Kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo ilikuwa kazi ya Enzi ya Neema, hatua ya kwanza katika kazi ya ukombozi, na sasa kwa kuwa Mungu Amemkomboa mwanadamu kutoka msalabani, Hatekelezi kazi hiyo kamwe. Ikiwa katika siku za mwisho “Mungu” sawa na Yesu Angeonekana, Ambaye Anaponya wagonjwa, Anafukuza mapepo na Anayesulubiwa kwa ajili ya wanadamu, “Mungu” huyo, japo Analingana na maelezo ya Mungu katika Biblia, na rahisi kwa mwanadamu kukubali, Hangeweza, katika kiini chake, kuwa mwili uliovaliwa na Roho wa Mungu, bali na roho mwovu. Kwani ni kanuni ya kazi ya Mungu kutorudia Alichokikamilisha. Hivyo basi kazi ya kupata mwili wa Mungu kwa mara ya pili ni tofauti na kule kwa kwanza. Katika siku za mwisho, Mungu Anafanikisha kazi ya kushinda katika mwili wa kawaida; Haponyi wagonjwa, Hatasulubishwa kwa ajili ya mwanadamu, ila tu Ananena maneno katika mwili, Anamshinda mwanadamu katika mwili. Ni mwili kama huo tu ndio mwili wa Mungu katika mwili; ni mwili kama huo tu ndio unaoweza kukamilisha Kazi ya Mungu katika mwili.
Ikiwa katika hii hatua Mungu mwenye mwili Anapitia ugumu au Anatekeleza huduma Yake, Anafanya hivyo ili kukamilisha maana ya kupata mwili, kwani huku ndiko Mungu kupata mwili kwa mara ya mwisho. Mungu Anaweza kuwa mwili mara mbili tu. Hakuwezi kuwepo mara ya tatu. Kuwa mwili kwa mara ya kwanza Alikuwa ni wa kiume, wa pili ni wa kike, na kwa hivyo sura ya mwili wa Mungu imekamilika katika akili za mwanadamu; aidha, huku kuwa mwili mara mbili tayari kumemaliza kazi ya Mungu katika mwili. Mara ya kwanza, Mungu mwenye mwili Alikuwa na ubinadamu wa kawaida, ili kukamilisha maana ya kupata mwili. Mara hii vilevile Ana ubinadamu wa kawaida ila maana ya huku kupata mwili ni tofauti: ni kwa kina, na kazi Yake ni ya umuhimu mkubwa. Sababu ya Mungu kuwa mwili tena ni kukamilisha maana ya kupata mwili. Mungu Akiikamilisha kabisa hii hatua ya kazi Yake, maana nzima ya kupata mwili, yaani, kazi ya Mungu katika mwili, itakuwa imekamilika, na hakutakuwa na kazi nyingine ya kufanywa katika mwili. Yaani, tangu sasa Mungu Hatawahi tena kuja katika mwili kufanya kazi Yake. Ni kwa kuokoa na kumfanya mwanadamu kuwa mkamilifu pekee ndiko Mungu Hufanya kazi ya kupata mwili. Kwa maneno mengine, si jambo la kawaida kwa Mungu kuwa na mwili, ila tu ni kwa minajili ya kazi. Kwa kuja kufanya kazi Akiwa kwenye mwili, Anamwonyesha Shetani kuwa Mungu ni mwili, mtu wa kawaida—lakini Anaweza kuitawala dunia kwa ushindi, Anaweza kumshinda Shetani, kumkomboa mwanadamu na kumshinda mwanadamu! Lengo la kazi ya Shetani ni kuwapotosha wanadamu, ilhali lengo la Mungu ni kuwaokoa wanadamu. Shetani huwateka wanadamu katika shimo lisilo na mwisho, ilhali Mungu Huwaokoa kutoka humo shimoni. Shetani huwafanya wanadamu wote wamwabudu, ilhali Mungu Huwafanya wawe wafuasi wa utawala Wake, kwani Yeye ndiye Bwana wa viumbe wote. Kazi hii yote hutekelezwa kupitia Mungu kupata mwili mara mbili. Mwili Wake kimsingi ni muungano wa ubinadamu na uungu na huwa na ubinadamu wa kawaida. Kwa hivyo, bila Mungu kuwa mwili, Mungu Asingeweza kufikia matokeo katika ukombozi wa mwanadamu, na bila ubinadamu wa kawaida wa mwili Wake, kazi Yake katika mwili bado haingefikia matokeo. Kiini cha kupata mwili kwa Mungu ni kwamba lazima awe na ubinadamu wa kawaida; kwani ingekuwa vinginevyo, ingekuwa kinyume na madhumuni asili ya Mungu ya kupata mwili.
Kwa nini Ninasema kuwa maana ya kupata mwili haikukamilishwa katika kazi ya Yesu? Ni kwa sababu Neno halikuwa Mwili kikamilifu. Kilichofanywa na Yesu kilikuwa tu sehemu moja ya kazi ya Mungu katika mwili; Alifanya tu kazi ya ukombozi na Hakufanya kazi ya kumpata mwanadamu kikamilifu. Kwa sababu hii, Mungu Amekuwa mwili mara nyingine tena katika siku za mwisho. Hatua hii ya kazi, pia inafanywa katika mwili wa kawaida, ikifanywa na mwanadamu wa kawaida kabisa, ambaye ubinadamu wake haupiti mipaka ya ubinadamu. Kwa maneno mengine, Mungu Amekuwa mwanadamu kamili, na ni mtu ambaye utambulisho wake ni ule wa Mungu, mwanadamu kamili, mwili kamili, Ambaye Anatekeleza kazi. Katika jicho la mwanadamu, Yeye ni mwili tu ambao haujapita mipaka ya ubinadamu hata kidogo, mwanadamu wa kawaida kabisa Anayeweza kuzungumza lugha ya mbinguni, Ambaye Haonyeshi ishara za kimiujiza, Hafanyi miujiza, sembuse kuweka wazi ukweli wa ndani kuhusu dini katika kumbi kuu za mikutano. Kazi ya kupata mwili kwa mara ya pili inaonekana kwa wanadamu kuwa tofauti kabisa na ile ya kwanza, kiasi kwamba kazi hizi mbili zinaonekana kutokuwa na uhusiano wowote, na hakuna chochote katika kazi ya kwanza kinachoweza kuonekana wakati huu. Japo kazi ya kupata mwili kwa mara ya pili ni tofauti na ile ya kwanza, hili halithibitishi kuwa chanzo Chao si kimoja na sawa. Iwapo chanzo Chao ni kimoja inategemea aina ya kazi iliyofanywa na miili na si katika maumbo Yao ya nje. Katika hatua tatu za kazi Yake, Mungu Amekuwa mwili mara mbili, na mara zote kazi ya Mungu kuwa mwili inaanzisha enzi mpya, inaanzisha kazi mpya; kuwa mwili kwa mara ya kwanza na pili kunakamilishana. Macho ya wanadamu hayawezi kugundua kuwa hii miili miwili kwa kweli imetokana na chanzo kimoja. Ni wazi kwamba hili liko nje ya uwezo wa macho ya wanadamu au akili za wanadamu. Ila katika kiini Chao, ni miili sawa, kwani kazi Yao inatokana na Roho mmoja. Iwapo hii miili miwili inatokana na chanzo kimoja haiwezi kuamuliwa kutokana na enzi na sehemu Ilipozaliwa, au vigezo vingine kama hivyo, ila kwa kazi ya uungu iliyoonyeshwa Nayo. Kupata mwili wa pili hakufanyi kazi yoyote iliyofanywa na Yesu, kwani kazi ya Mungu haifuati makubaliano, lakini kila wakati inafungua njia mpya. Kupata mwili wa pili hakulengi kuongeza au kuimarisha maono ya kupata mwili wa kwanza katika akili za watu, ila kuutimiza na kuukamilisha, kuongeza kina cha wanadamu kumwelewa Mungu, kuvunja sheria zote ambazo zipo katika mioyo ya watu, na kufuta picha za uongo kuhusu Mungu mioyoni mwao. Ni wazi kuwa hakuna hatua yoyote ya kazi ya Mungu mwenyewe inaweza kumpa mwanadamu ufahamu kamili wa Mungu; kila mojawapo inatoa kwa sehemu tu, si ufahamu mzima. Japo Mungu Ameonyesha tabia Yake kikamilifu, kwa sababu ya upungufu wa ufahamu wa wanadamu, ufahamu wake kuhusu Mungu si kamili. Haiwezekani, kutumia lugha ya wanadamu, kueleza tabia nzima ya Mungu; basi hatua moja tu ya kazi Yake itamwelezaje Mungu kikamilifu? Anafanya kazi katika mwili kwa kujisetiri katika ubinadamu Wake wa kawaida, na mtu anaweza kumjua tu kupitia kwa maonyesho ya uungu Wake, si kupitia kwa umbo Lake la kimwili. Mungu Anakuja katika mwili kumruhusu mwanadamu Amjue kupitia kazi Zake mbalimbali, na hakuna hatua mbili za kazi Yake zinafanana. Ni kwa njia hii tu mwanadamu anaweza kuwa na ufahamu kamili wa kazi ya Mungu katika mwili, si kwa kujifunga katika kipengele kimoja tu. Japo kazi ya hii miili miwili iliyopatikana ni tofauti, kiini cha hii miili, na chanzo cha kazi Yao vinafanana; ni kwamba tu Ipo ili kutekeleza hatua mbili tofauti za kazi, na inatokea katika enzi mbili tofauti. Licha ya jambo lolote, miili ya Mungu katika mwili inashiriki kiini kimoja na asili moja—huu ni ukweli ambao hauwezi kupingwa na yeyote.
Tanbihi:
a. Maandishi ya awali hayana kauli “kazi ya.”
Soma zaidi: Kujua Kanisa la Mwenyezi Mungu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni